Tuesday, February 18, 2014

Bunge lagawanyika!

Dodoma. Bunge Maalumu la Katiba, linaanza leo mjini hapa, huku kukiwa na mpasuko mkubwa miongoni mwa wajumbe, unaotokana na misimamo tofauti.
Kipengele kinachowagawa wajumbe hao ni Muundo wa Serikali uliopendekezwa katika Rasimu ya Katiba.
Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, iliyokutana kwa siku mbili Mjini Dodoma imeondoka na msimamo wa kutaka wajumbe wake wa bunge hilo kutetea hoja ya Serikali mbili huku Chadema na CUF vinataka Serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila hivi karibuni alikaririwa akitishia kwenda mahakamani kuzuia mchakato mzima wa Katiba hadi iundwe Serikali ya Tanganyika.
Msimamo wa CCM
Akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya CCM Mjini Dodoma jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema msimamo wa chama chake haujabadilika na kwamba wanafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa Tanzania inabaki na mfumo wa Serikali mbili.
“Hatuwezi kukataa mawazo ya watu wengine, lakini kikubwa ambacho tunakisimamia ni kuhakikisha kuwa tunabaki na Serikali mbili na ndiyo maana tumezungumza na wajumbe wa NEC na leo (jana), tunakutana na wabunge wetu wa Bunge la Muungano na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar,” alisema Nape.
Kuhusu kero zinazolalamikiwa na pande zote, alisema CCM inafahamu kero nyingi na kwamba upande wa Bara kuna kero nane na Zanzibar idadi kama hiyo.
“CCM imetengeneza mfumo mzuri wa kuziondoa kero hizo ndani ya Serikali mbili siyo kama wenzetu ambao wamebuni Serikali tatu eti iwe dawa ya kumaliza kero hizo kitu ambacho hakiwezekani,” alisema huku akiwataka wajumbe na Watanzania kwa jumla, kulumbana kwa hoja badala ya kupiga kelele.
Malecela aipinga CCM
Hata hivyo, kada mkongwe aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, John Malecela alitofautiana na msimamo huo akisema si sahihi kwa viongozi kuwatungia wananchi Katiba kama inayoonekana kufanywa na baadhi yao.
Akizungumza kwa simu kutoka Nairobi, Kenya, Malecela alisema: “Kama tuliona inafaa kuwatungia wananchi Katiba, hakuna ulazima wa kuwataka maoni yao. Mimi ni kiongozi na Katiba hii ni ya wananchi, nisingependa kutoa maelekezo ya nini kifanyike, kama viongozi wengine wanavyofanya.

No comments:

Post a Comment