Wednesday, February 19, 2014

BUNGE LA KATIBA VITUKO TUPU.

Mh.Pandu Amir Kificho

MWENYEKITI wa CHADEMA, Freeman Mbowe ambaye pia ni mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, jana alinusuru mchakato wa uchaguzi wa mwenyekiti wa muda baada ya kuibuka vituko.
Mbowe katika ushauri wake alitaka mchakato huo uanze upya kwa karatasi za kura kugawiwa kwa utaratibu makini ili kila mmoja apige kura huku milango ikiwa imefungwa.
Ushauri wake ulikubaliwa na mwenyekiti wa kikao hicho ambapo mchakato ulifanyika upya kwa usimamizi mkali wa polisi, huku Bunge likiahirishwa kwa robo saa kutoa fursa ya kura kuhesabiwa.
Awali vituko kejeli na malumbano vilitawala zaidi uchaguzi huo wa Bunge lililoanza vikao vyake jana mkoani hapa.
Dalili za kuvurugika kwa uchaguzi huo zilianza kuonekana mapema kutokana na idadi kubwa ya wajumbe kusimama na kuwasha vipaza sauti bila kufuata taratibu walizoambiwa mapema.
Katika uchaguzi huo Mheshimiwa Pandu Amir Kificho alishinda nafasi ya Mwenyekiti wa muda wa Bunge la Katiba baada ya kupata kura 393 sawa na 69.19% ya kura 558 zilizopigwa na kuwaacha kwa mbali Costa Mahalu na Magdalena Rwebangira ambao wamepata kura 84 kila mmoja ambazo ni sawa na 14.79%
Kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya katiba, mwenyekiti huyo wa muda atakuwa na jukumu la kuandaa na kupitisha kanuni za Bunge hilo zitakazotumika katika mijadala mbalimbali.

No comments:

Post a Comment