Thursday, May 3, 2012

SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI DUNIANI!-Uhuru wa waandishi bado kifungoni.

 Ikiwa leo ni maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari duniani bado changamoto ni nyingi kwa fani hii na bado safari ni ndefu,ambapo uhuru na usalama wa waandishi wa habari umeonekana kuwa mdogo na usiowapa uhakika wa kufanya kazi zao kwa ufanisi.Msemaji wa mwenyekiti wa waandishi wa habari wasiojali mipaka, kanda ya Ujerumani Michael Rediske amesema waandishi wa habari wanapaswa kuwa ugani, lakini aghalabu wanashambuliwa, hasa na serikali zao, changamoto nyingine ni rushwa, na umasikini ambavyo kwa pamoja  vimezorotesha uhuru wa vyombo vya habari.

Katika baadhi ya nchi kama Eritrea na Korea ya Kaskazini uhuru wa vyombo vya habari umeondolewa kabisa na waandishi wa serikali pekee wameruhusiwa kuandika habari ili kuisifu serikali na kufuata matakwa yake.



Hata hivyo viwango vya uhuru wa vyombo vya habari vinatafautiana sana baina ya nchi na nchi. Kazi ya waandishi nchini Tunisia sasa siyo ya hatari kama ilivyokuwa hapo awali. Lakini nchini Syria waandishi wa habari kadhaa wameuawa tokea mapigano yaanze nchini humo. Mazingira yanayowakabili waandishi wa habari nchini Syria leo ni hatari sawa na yale yaliyojiri nchini Iraq katika miaka ya nyuma.

 Lakini hali ni hivyo hivyo huko Somalia na sehemu nyingine za Afrika ambazo tawala za serikali zimekuwa hazitaki kukosolewa wala mabaya yao kuanikwa hadharani kwa kalamu.
 Lakini pia katika nchi za uchina, nchi za kiarabu hususani zile zilizopitiwa na mapinduzi ya umma na nchi nyingi za Kiafrika na Asia ambazo zimejiita za kidemikrasia ingawa zimeshindwa kufanya hivyo katika uhuru wa vyombo vya habari.Waandishi katika nchi nyingi za dunia ya tatu wameshambuliwa wakati wa matukio ya uchaguzi na kuripoti matukio ya rushwa na ubadhilifu wa mali ya umma unaofanywa na viongozi wa kisiasa.

Rushwa na umasikini ni changamoto nyingine hasa kwa nchi zinazoendelea, waandishi wengi wameshawishiwa kupokea rushwa ili kuandika habari zenye kupendelea upande fulani na kuharibu fani zao, lakini hasa hili limechangiwa na umasikini unaotokana na maslahi duni wanayopata katika kazi hiyo.


SULUHISHO.

Serikali, iboreshe sera na sheria zenye kulinda maslahi na uhuru wa waandishi hasa dhidi ya waajiriwa wa serikali wenye nguvu za dola, pili ihakikishe maslahi ya waandishi yanasimamiwa vyema ikiwa ni pamoja na kusimamia maslahi katika vyombo binafsi.

Wadau, washirikiane na waandishi wa habari na serikali kuhakikisha uhuru wa  vyombo vya habari na maslahi bora kwa waandiishi kupitia harakati binafsi namawazo na mipango thabiti ya mtu  mmoja mmoja au kikundi.

Waandishi, mwisho ni kwa waandishi wa habari wenyewe kuungana na kuimarisha umoja wao, kuibua mawazo na fikra zitakazosaidia uboreshaji wa sekta yao na kuichukulia fani ya uandishi wa habari kama wito na hivyo kuifanya kwa uvumilivu na ujasiri bila ya kurudishwa nyuma na vikwazo vinavyowakabili.

"Uhuru wa Vyombo vya Habari Unasaidia Kubadili Jamii!!".



 
 
 
Akisisitiza umuhimu wa kuiadhimisha siku ya leo ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, msemaji wa mwenyekiti wa waandishi wasiojali mipaka , kanda ya Ujerumani bwana Rediske ameeleza: "Ni siku ya kutanabahisha juu ya matatizo, juu ya hali ya uhuru wa vyombo vya habari, kwa kutilia maanani kwamba katika theluthi mbili ya nchi duniani, hakuna uhuru wa vyombo vya habari." Alitolea mfano wa Korea ya Kaskazini ambako hakuna waandishi wa kujitegemea, na kwa sababu hiyo hawakamatwi na Eritrea ambako waandishi wa habari wengi wanatiwa ndani.
 

No comments:

Post a Comment