Monday, October 22, 2012

MWAKYEMBE AKABIDHIWA RIPOTI YA BANDARI

DAR ES SALAAM-TANZANIA, WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amekabidhiwa ripoti ya uchunguzi wa utendaji kazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), huku akitoa onyo kali kwa vigogo waliokwepa kuhojiwa na kamati kwa visingizio mbalimbali akisema ni lazima watahojiwa tu. Dk. Mwakyembe alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo yenye kurasa 285 na Mwenyekiti, Wakili Benard Mbakileki, na kuongeza kuwa kama suala analotaka kuhojiwa mhusika linahusu polisi, atapelekwa mbele ya jeshi hilo. Waziri Mwakyembe alitoa kauli hiyo baada ya Wakili Mbakileki kueleza kuwa baadhi ya watu muhimu TPA waliotakiwa kuhojiwa walikwepa kwa visingizio mbalimbali ikiwamo kuuguliwa, kufiwa na wengine kuzima simu kabisa. Akijibu hoja hiyo, Dk. Mwakyembe alisema: “Kama walidhani kukwepa kamati ndio mambo yameisha, wanajidanganya. Watakuja kujibu mbele yangu na kama mambo yanahusu polisi tutawapeleka, hatutaacha mtu.” Aliongeza kuwa kamati hiyo imefanya kazi ya kizalendo na kuahidi mambo yote iliyopendekeza watayafanyia kazi hatua kwa hatua, ili kuboresha bandari hiyo. “Niwahakikishie hii kazi mliyoifanya haitakwenda bure, hadi kufikia Desemba mwaka huu, tutakuwa tumeyafanyia kazi mambo yote mliyopendekeza. Tutataka kuipa bandari sura mpya, kwa sasa inakosa ufanisi…tutakuja na uamuzi ambao hakitadokolewa kitu, kwani watakaodokoa, nao watadokolewa, kwani tusipofanya uamuzi huo hatutaikomboa nchi yetu,” alisema. “Tulikuwa tunasikia habari za Twiga kusafirishwa kwenye ndege watu wakashangaa, lakini pale bandarini kontena na ukubwa wake linayeyuka. Mwaka juzi yaliyeyuka makontena 10, mwaka jana 26 na mwaka huu mawili na mambo yanatufanya tusiaminike,” alisema. Waziri Mwakyembe alibainisha kuwa kutokana na hali hiyo, watafanya kazi kwa gharama yoyote, bila kumwonea mtu, ili kurekebisha bandari hiyo aliyoeleza kuwa iwapo ingesimamiwa vizuri nchi ingeweza kuendesha mambo mengi. Aidha, alibainisha kuwa tangu kamati hiyo ilipoanza kufanya kazi, baadhi ya nchi jirani zimeanza kurejesha imani na bandari hiyo zilikemo Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Rwanda na Burundi. Aliongeza kuwa iwapo baadhi ya watu wanakerwa na mabadiliko ndani ya TPA, waondoke kwani mjini kuna kazi nyingi za kufanya. Pamoja na mambo mengine, Mwakyembe aliomba wapatiwe muda wa kuipitia ripoti hiyo kwa umakini na kwamba kila hatua watakuwa wakitoa taarifa kwa umma.(Chanzo:Bongonewztz)

No comments:

Post a Comment