Monday, March 3, 2014

Mwelekeo mpya bungeni, Pinda atoa hoja .

Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana alifanikiwa kutuliza hali ya hewa bungeni baada ya kutoa mapendekezo yaliyoungwa mkono na pande zote zilizokuwa zinavutana kuhusu kupitisha baadhi ya vifungu vya Kanuni za Bunge la Katiba.
Katika mapendekezo yake yaliyoungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu wa CCM -Zanzibar, Vuai Ali Vuai, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Pinda alisema: “Nataka kuwaomba wenzangu wote kwenye maeneo hayo (yenye malumbano) tukiwa tunayapitia kama hatutaelewana tuyaache kwa muda na kumwomba Mwenyekiti aunde timu ya watu wazima na wenye busara wajaribu kuyatazama. “Tujadiliane, tushindane kwa lugha za staha, tusitumie lugha inayoweza kukasirisha. Isiwe mimi nimesema, mimi nimesema...”
Waziri Mkuu, aliwataka wajumbe wajiepushe na lugha za kuudhi ambazo zinaweza kukwamisha upatikanaji wa Katiba Mpya.
Pinda alilazimika kuingilia kati baada ya kutokea mgawanyiko mkubwa wa namna ya kupiga kura kupitisha vifungu vya rasimu.
Akiunga mkono ushauri huo, Mbowe alisema Bunge limejaa hisia za hofu ndani na nje, jambo ambalo linatia wasiwasi wa kupatikana kwa Katiba Mpya. Alisema iwapo wajumbe watashirikiana na kuweka kando masilahi ya vyama, idadi yao katika makundi, Katiba inaweza kupatikana.
Vuai alionya kuhusu matumizi ya lugha za kuudhi huku Profesa Lipumba akiwataka wajumbe kuzingatia masilahi ya Taifa kama alivyoagiza Rais Jakaya Kikwete na kutengeneza Katiba ya Watanzania wote bila ya kujali masilahi binafsi.
Upigaji kura bungeni vita
Awali, mjadala wa utaratibu wa upigaji kura katika Bunge hilo ulichukua sura mpya baada ya kudaiwa kuwapo ushawishi unaohusisha utoaji wa bahasha ili kutaka kuungwa mkono katika misimamo inayokinzana.
Habari zilizopatikana zilidai kuwa watuhumiwa katika sakata hilo ni baadhi ya wajumbe ambao ni mawaziri na mbunge mmoja wa CCM. Vigogo hao wanadaiwa kuwashawishi wajumbe ambao hawatokani na vyama vya siasa ili kupitisha agenda ya kura ya wazi kirahisi.
Akiandika kwenye ukurasa wake wa Facebook, Mjumbe wa Bunge hilo, Julius Mtatiro ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF, alisema: “Jaribio la kuzuia kura ya siri limechukua njia za aibu, baada ya CCM kutumia fedha kushawishi wajumbe.”
Katika ujumbe huo ambao alikiri kuuandika, Mtatiro aliwataja wajumbe watatu ambao ni mawaziri kuwa waliwakaribisha wajumbe kwenye makazi yao na “kuwaandalia chakula cha kutosha, vinywaji vya kutosha na viburudisho vingine, huku wakipewa bahasha za nauli baada ya vikao hivyo vya siri.” Mmoja wa waliotajwa ni Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe aliyedaiwa kuwaalika wawakilishi wa wafugaji na kuwapa chakuka na bahasha.
Akijibu tuhuma hizo, pamoja na kukiri kuwakaribisha baadhi ya wajumbe na kula nao chakula, alikana tuhuma za kuwahonga ili waunge mkono msimamo wa chama hicho. Alisema Mtatiro amemdhalilisha, hivyo anawasiliana na mwanasheria wake ili kumfikisha mahakamani.

Chanzo: Mwananchi.

No comments:

Post a Comment