Sunday, March 30, 2014

Urais wamponza Sitta

 Samuel Sitta avuruga kanuni kutaka urais 2015

MWENENDO wa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, umeanza kutiliwa shaka huku baadhi ya wajumbe wenzake wakidai anateswa na dhambi ya unafiki.
Sitta, ambaye aliongoza Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano kwa uwezo mkubwa chini ya falsafa yake ya viwango na kasi, alichaguliwa kwa kura nyingi kuongoza Bunge la Katiba akiahidi kuendeleza falsafa hiyo.
Hata hivyo Sitta ameanza kushindwa kuitekeleza ahadi hiyo baada ya kuruhusu kufinyangwa kwa kanuni za Bunge pamoja na kufanya uteuzi wa wajumbe wa kamati ya uongozi akiwapendelea wajumbe kutoka CCM.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa kuyumba huko kwa Sitta kunachangiwa na ndoto zake za kutaka kuwania urais mwaka 2015, hivyo anatafuta kuungwa mkono na CCM.
Sitta anatafuta kuungwa mkono na CCM kwakuwa chama hicho mwaka 2010 mara baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu kilimtosa kuwania uspika kwa madai ni zamu ya mwanamke.
Miongoni mwa sababu zilizokuwa zikitajwa chinichini ni kuwa kiongozi huyo wakati akiwa spika aliruhusu mijadala iliyozusha makundi ndani ya chama na serikali.
Katika utawala wake Sitta, aliunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza zabuni iliyoipa ushindi wa kuleta mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura Kampuni ya Richmond, iliyokuwa ikilipwa sh milioni 152 kwa siku.
Kamati teule hiyo iliyokuwa chini ya Dk. Harrison Mwakyembe, ilitoa ripoti iliyobaini kulikuwa na utata katika kuipa ushindi zabuni ya Richmond, waliodai ni ‘hewa’ na yenye mkono wa ‘bwana mkubwa’.
Kashafa hiyo ilimfanya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu baada ya kuguswa na kashfa hiyo.
Hata hivyo mchakato huo ulifungwa na Sitta, katika mazingira ya aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM), aliyeguswa pia na kashfa hiyo akitaka iundwe tume huru ya majaji watatu kuchunguza sakata hilo.
Tangu hapo Sitta, amekuwa kwenye uahasama mkubwa na makada wenzake pamoja na chama ambacho kinaamini utawala wake ndio uliozalisha wapinzani wengi bungeni hivi sasa.
Kutokana na dhana hiyo, Sitta hivi sasa amekuwa akifanya mambo yanayoonekana kutafuta huruma ya chama chake ambapo pia nusuru kisimpe ridhaa ya kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, nafasi iliyokuwa ikitajwa kukaliwa na Andrew Chenge.
Miongoni mwa mambo anayoshutumiwa kuyafanya Sitta ni kuwakemea wenzake kwa ufisadi wanaoufanya wanapotoa fedha kwenye harambee na shughuli za kijamii ilhali naye amekuwa akipita makanisani kuomba huruma ya wananchi.
Sitta pia analaumiwa kwa kuruhusu uvunjwaji wa kanuni za kuliongoza Bunge kwa kuruhusu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba awasilishe rasimu ya katiba kabla ya Rais Jakaya Kikwete.
Inadaiwa alifanya hivyo ili kumtengenezea mazingira Rais Kikwete, kujibu mapendekezo yaliyokuwamo kwenye Rasimu ya Katiba ili kuipa ahueni CCM inayopinga mfumo wa serikali tatu uliopendekezwa kwenye rasimu.
Sitta pia anadaiwa kufanya uteuzi wa wajumbe watatu kati ya watano kuingia katika kamati ya uongozi ambayo inaongozwa na wenyeviti 12 kutoka CCM.
Miongoni mwa walioteuliwa kwenye kamati hiyo ni Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye alikataa uteuzi huo huku akimlaumu Sitta kwa kufanya uteuzi unaoangalia zaidi masilahi ya chama chake kuliko taifa.
Baadhi ya wajumbe hususan wapinzani wanadai Sitta anayumbishwa na Chama chake Cha Mapinduzi (CCM), hivyo kufikia hatua ya kuzivunja kanuni za Bunge na kuibua mivutano.
Udhaifu wa Sitta
Baadhi ya wajumbe wa upinzani wanasema tabia ya kutokuwa na msimamo aliyoanza kuionyesha Sitta hivi sasa kwa kufuata matakwa ya chama chake bila kujali uzito wa hoja husika kumemvunjia heshima.
Hoja yao ni kuwa falsafa ya ‘Kasi na Viwango’ aliyoitangaza ameshindwa kuionyesha katika Bunge Maalumu kiasi cha kuyumbisha mchakato wa mijadala bungeni.
Pia ndani ya CCM, Sitta anatazamika kwa sura mbili. Mosi, washindani wake kisiasa wanadai anaongoza Bunge hilo kwa kuwasikiliza zaidi wapinzani ili kujijengea uhalali wa kugombea urais 2015.
Kundi la wafuasi wake, lenyewe linaona kama Sitta yuko imara kusimamia mchakato wa Katiba isipokuwa anakwazwa na mahasimu wake ndani ya chama wanaomuundia zengwe aonekane dhaifu.
Kangi Lugola (CCM), alikuwa wa kwanza kumtahadharisha Sitta kuhusiana na uongozi wake, akisema nafasi yake ni sawa na Jaji wa Mahakama Kuu aliyepelekewa mtuhumiwa wa mauaji amhukumu.
“Sitta ndiye amepewa jukumu la kuhakikisha anasimamia mchakato huu ili wananchi wapate Katiba mpya na nzuri, kushindwa kufanya hivyo wananchi wataondoa imani kwake na chama,” alisema Lugola ambaye pia ni Mbunge wa Mwibara.
Lugola aliongeza kwamba licha ya CCM kuwa na wajumbe wengi katika Bunge hilo lakini Sitta alichaguliwa kwa kuaminiwa kutokana na utashi wake wa kisiasa, hivyo anapaswa kutumia busara.
Naye Godbless Lema (CHADEMA) alimtaka Sitta kuwa makini na kila iana ya ushauri anaopewa na wenzake ndani ya CCM, kwamba mwingine una lengo la kumchafulia rekodi yake.
Lema ambaye pia ni Mbunge wa Arusha Mjini, alisema kuwa wabaya wa Sitta wamekuwa wakijidai kumshauri hata mambo ambayo baadaye yanaleta matatizo kwa lengo la kutaka kuonyesha kuwa alishindwa kusimamia mchakato wa kuandika katiba.
“Wako wabaya wako wanataka mchakato huo usifanikiwe ili ionekane ulishindwa kusimamia wananchi wapate katiba, hivyo waseme haufai hata kugombea urais,” alisema Lema bungeni.
Naye  John Shibuda, anasema Sitta anatafunwa na dhambi ya unafiki wake ambao hauwezi kumfikisha katika anachokifikiria.
Shibuda alisema Sitta amejikuta wakati mwingine akifanya uamuzi wa kuibeba CCM ili kujinafikisha aonekane ni kada mwaminifu na wakati huo huo anataka kujijengea ushujaa ili katiba mpya ipatikane, atumie turufu hiyo kujipigia debe la urais 2015.
Wiki iliyopita Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema Sitta ni dhaifu na ndiyo maana anashindwa kuongoza Bunge Maalumu la Katiba kwa sababu ya kuegemea zaidi kwenye chama chake.
Dk. Slaa alisema uongozi wa Sitta bungeni utasababisha mivurugano mikubwa na kutoelewana baina ya wajumbe waliopewa jukumu la kuandika Katiba inayopendekezwa, ambayo itakwenda kupigiwa kura ya maoni na wananchi.

Sitta amekuwa akilalamikiwa na baadhi ya wajumbe tangu siku ya kwanza alipokalia kiti hicho kuwa anavunja kanuni alizotamba kuzisimamia kwa kasi na viwango.

No comments:

Post a Comment