Monday, March 3, 2014

‘Pandu Kificho ametusaliti’

Zanzibar. Mwenyekiti wa Muda wa Bunge la Katiba, Pandu Ameir Kificho amekiri kuwasilisha waraka kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba na kupendekeza Zanzibar na Tanganyika kuwa na mamlaka huru, hatua ambayo imezua malalamiko miongoni mwa makada wa chama hicho ambao wamesema huo ni usaliti.
Akizungumza kwa simu kutoka Dodoma, Kificho ambaye pia ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), alisema kimsingi waraka huo ulilenga kuipa nguvu Zanzibar kushughulikia mambo yasiyo ya Muungano ili kujiimarisha kiuchumi.
Kauli ya Kificho inakuja wakati baadhi ya wajumbe wa CCM kutoka Zanzibar wakiitisha mkutano na kutoa tamko la kumshutumu kwa kutoa mapendekezo hayo, wakisema ni kinyume na msimamo wa chama hicho.
Kificho alionyesha kushangazwa na madai kuwa mapendekezo hayo yaliyoandaliwa na watu wanne ambayo ameyasaini si msimamo wa BLW.
“Tatizo lililopo ni tafsiri ya kila mmoja anapousoma waraka huo, hakuna sehemu tuliyoandika tunataka Serikali tatu, mamlaka huru maana yake kila upande uwe na uwezo wa kushughulikia mambo yake yasiyo ya Muungano na kujijenga kiuchumi, ikiwa ni pamoja Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Kiislamu ya Kimataifa (OIC) na siyo kuunda dola,” alifafanua Spika Kificho.
Alisisitiza kuwa angependa mambo ambayo hayamo katika orodha ya Muungano yaendeshwe na Zanzibar bila ya kuwekewa vikwazo mahali popote.
Madai hayo ni dalili za wazi za mgawanyiko baina ya wajumbe wa CCM ambao wameanza kuonyesha makundi mawili yenye misimamo tofauti.
Kundi linalomshutumu Kificho, linawajumuisha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Juma Ali Shamhuna, Waziri Kiongozi mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Spika wa BWZ, Ali Abdallah Ali.
Jana, kundi hilo lilimtuhumu Kificho kuwa hakuwashirikisha wenzake katika mapendekezo Serikali tatu aliyoyawasilisha kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wakisema  Baraza la Wawakilishi, kama taasisi, halikutoa msimamo wa pamoja.
Hata hivyo, mtazamo huo wa BLW unatofautiana na ule wa Kificho uliowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Othman Masoud Othman, ukipendekeza Serikali tatu.
“Kwa vile mfumo wa Serikali mbili uliopo sasa hauwezi kujenga Muungano utakaohimili mabadiliko ya kisiasa na kwa vile umejaribiwa na kuthibitishwa kuwa umeshindwa kujenga Muungano imara, uachwe katika kuendesha Muungano wa Tanzania,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo ya Othman.
Jana asubuhi, zaidi ya wajumbe 10 wa Baraza la Wawakilishi akiwamo Shamhuna, Nahodha na Ali waliitisha mkutano wa waandishi wa habari mjini Dodoma na kumtupia lawama Kificho wakisema; “Amewasaliti katika mchakato huo wa Katiba.”

No comments:

Post a Comment