Monday, December 31, 2012

URAIS 2015-CHADEMA YAGAWANYIKA

DAR ES SALAAM-TANZANIA,
SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kumtangaza Dk Willibrod Slaa kuwa ndiye mgombea wa urais mwaka 2015 kwa tiketi ya chama hicho, makada wa chama hicho wamegawanyika baadhi wakimponda na wengine kumuunga mkono. Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya makada wa chama hicho walisema mwenyekiti wao amekosea kumtangaza mgombea kabla ya wakati, huku wanaomuunga mkono wakisema hajakosea kwa sababu hatua hiyo itasaidia kuondoa makundi ndani ya chama hicho. Juzi, Mbowe akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Karatu mkoani Arusha, alisema Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willibrod Slaa atapewa fursa ya kuwania tena urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015, huku mwenyewe akijiweka kando kuwania nafasi hiyo Hata hivyo, Dk Slaa alipoulizwa iwapo ana nia ya kuwania nafasi hiyo alihoji: “Kwani mwaka 2010 nilijitangaza mwenyewe,? Iwapo wanachama wa Chadema watanipendekeza nitafikiria kufanya hivyo.” Mwasisi wa chama hicho Edwin Mtei, Wajumbe wa Kamati Kuu; Profesa Mwesiga Baregu na Dk Kitila Mkumbo, Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa Bavicha John Heche na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema walitoa maoni yanayopingana kuhusu kauli hiyo ya Mbowe. Wanaounga mkono Mtei alisema anaunga mkono kauli ya Mbowe akisema kiongozi huyo hajakosea kumtangaza Dk Slaa kuwania urais mwaka 2015. “Ninaunga mkono Dk Slaa kuwania tena nafasi ya urais mwaka 2015. Mwenyekiti amemtangaza baada ya kupata baraka ya vikao vya chama,” alisema Mtei. Ingawa Mtei hakuwa tayari kusema ni kikao gani kilichopitisha jina la Dk Slaa kuwania nafasi hiyo, alisisitiza: “Kuna vikao vya Kamati Kuu vimefanyika hivi karibuni, vinaweza kuwa vimefanya uamuzi huo. Mwenyekiti hawezi kuzungumza jambo bila baraka za vikao vya chama.” Hata hivyo, kauli hiyo ya Mtei inapingana na ile aliyoitoa Oktoba 6, mwaka huu baada ya Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini kutangaza kutogombea tena ubunge badala yake kusema anataka kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2015. Mtei alisema hatua ya Zitto kutangaza kuwania urais mapema kungesababisha mzozo na mpasuko ndani ya chama hicho. Mtei alisema amekuwa akimshauri Zitto mara kwa mara kuhusu hatua yake hiyo akimtaka kuwaunganisha wana Chadema na siyo kuwagawa au kuwavuruga. “Hakuna shida kuonyesha hisia, lakini unatengeneza mzozo mkubwa sana ukitangaza sasa. Mimi nimeshamshauri sana Zitto, ahakikishe anakiunganisha chama na siyo kukigawa wala kukivuruga.” Alisema mbunge huyo kutangaza kutogombea tena ubunge na badala yake kujipanga kuwania urais mwaka 2015 kumekuja mapema mno na kuonya kuwa itaibua mzozo ndani ya Chadema. Mtei ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu enzi za utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, alisema kwamba wakati mwafaka ukiwadia, Chadema kitaamua ni nani mwenye sifa za kugombea urais huku akisema kina utaratibu wake wa kuwapata wagombea mbalimbali wa uongozi. Hata hivyo, Zitto jana alikataa kuzungumzia suala hilo akisema: “Nimesikia hata mimi kwenye vyombo vya habari ila sina cha kuzungumza kuhusu hilo.” Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Heche alisema kauli hiyo Mbowe siyo yake binafsi, bali ni ya wananchi(CHANZO:MWANANCHI)

Saturday, December 22, 2012

TAIFA STARS VS CHIPOLOPOLO LEO.


DAR ES SALAAM-TANZANIA,
NAHODHA aliyeiwezesha Timu ya Taifa ya Zambia (Chipolopolo) kuandika historia ya kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka huu, Christopher Katongo leo anakiongoza kikosi hicho katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Timu ya Taifa (Taifa Stars) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katongo, mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka BBC mwaka huu, atakikabili kikosi cha Stars katika mechi hiyo ya kihistoria na pekee kwa aina yake kwa timu hizo mbili.
Hii ni mara kwa kwanza kwa Zambia inayoshika nafasi ya 34 kwa viwango vya ubora katika Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kucheza na Stars inayoshika nafasi ya 130, kama bingwa mtetezi wa mataifa ya Afrika.

Hata hivyo, mara ya mwisho kabla ya mchezo wa leo, zilikutana mwaka jana wakati wa michuano ya Kombe la Chalenji kwenye Uwanja wa Taifa, shukrani kwa bao la Felix Sunzu lililoipa ushindi wa bao 1-0 Zambia dhidi ya Stars.
Chipolopolo ilitwaa taji la Afrika baada ya kuifunga timu iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa kutokana na kuundwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa sehemu mbambali duniani, Ivory Coast.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Chipolopolo Patrice Beaunelle alisema haifahamu vizuri Tanzania kwa miaka ya karibuni, na kwa sababu hiyo anatarajia mchezo huo utakuwa mgumu na upinzani mkali.
Beaunelle alisema kwa vile, haifahamu vizuri Stars inayofundishwa na Kocha Kim Poulsem, atakipanga kikosi chake kamili wakiwamo baadhi ya chipukizi walioonyesha kiwango kinachovutia.

Mbali na Katongo, wengine watakaoshuka dimbani kuivaa Stars ni
Felix Katongo,Isaac Chansa, Francis Kasonde na Given Singuluma.
Pia anatarajia kuwasili wachezaji wengine waliochelewa kujiunga na wenzao, ambao ni Stophira Sunzu na Rainford Kalaba.

Kwa upande wake Kocha Poulsen atakayeshusha kikosi kitakachowakosa wachezaji wa kulipwa, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu amesema mchezo utakuwa mgumu kwa vile wanakutana na timu yenye uwezo mkubwa.
Pia hatakuwa na mshambuliaji wake nyota, John Bocco aliyeumia wakati wa mazoezi, kama ilivyo kwa Samata na Ulimwengu ambao tangu kuwasili wameshindwa kufanya mazoezi na wenzao kwa sababu ya kuwa majeruhi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Poulsen alisema pamoja na kukosekana kwa wachezaji hao bado ana matumaini ya kuisimamisha Zambia inayojiandaa kwenda kutetea taji lao nchini Afrika Kusini mwezi ujao.

"Naipongeza Zambia kwa kukubali kuja nchini kucheza mechi ya kirafiki, tuna kila sababu ya kujivunia lakini hilo halitatufanya tucheze kwa kuiogopa," alisema Poulsen.
"Natumaini mechi hii itatusaidia kujifunza mengi na pia itakuwa ni kipimo kizuri kwa timu yetu kwa ajili ya mechi mbalimbali zilizopo mbele yetu za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia pamoja na zile za mashindano ya CHAN.

"Nawaomba Watanzania wajitokeza kwa wingi na kutuunga mkono katika mchezo huu na kukosekana kwa Samata, Ulimwengu na Bocco isiwe sababu ya kutokutuunga mkono," alisema Poulsen.(CHANZO:MWANANCHI)

BARAZA LA USALAMA-UN LAIDHINISHA UVAMIZI WA KIJESHI MALI

NEW YORK-MAREKANI,Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa UN kwa pamoja wameidhinisha azimio la kupeleka vikosi vya kigeni kaskazini mwa Mali ili kupambana na Makundi ya kiislamu yenye msimamo Mkali yanayoshikilia eneo hilo tangu mwezi machi mwaka huu

Azimio hilo limepitishwa na Wanachama kumi na tano wa Baraza la usalama la umoja huo na kutoa muda wa kuchukua hatua za lazima kusaidia Serikali ya Mali kurudisha maeneo yanayokaliwa na Wapiganaji wa Kiislamu.

Hata hivyo pamoja na kupitishwa kwa Azimio hilo, Baraza limetaka kufanyika mazungumzo kati ya serikali na makundi ya wapiganaji ili kupata suluhu ya kisiasa nchini Mali.

Mataifa ya Afrika magharibi yamesema tayari yana vikosi 3300 vilivyo tayari kuingia Mali, kulijengea uwezo jeshi la Mali na kusaidia Operesheni za kijeshi nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti ya UN, takribani watu 400,000 wamepotea tangu kuzuka kwa machafuko hayo mwezi machi mwaka huu.

DK.MWAKYEMBE ATIMUA WENGINE 16 BANDARI.


Dk Mwakyembe atimua wengine 16 Bandari

DAR ES SALAAM-TANZANIA 
Baada ya kuwasimamisha viongozi saba, akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Ephraim Mgawe, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, ameendelea na juhudi za kutaka kuirejeshea hadhi mamlaka hivyo, na safari hii amewasimamisha kazi viongozi wengine 16.
Dk Mwakyembe aliyasema hayo jana alipozungumza na wafanyakazi wa mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam, akisema uamuzi wake umekuja baada ya kubainika kuwepo kwa matatizo mengi yanayokwamisha ufanisi wa shughuli za mamlaka hiyo.
Alisema Bodi mpya ya TPA ilikutana na kupitia taarifa ya uchunguzi na baada ya kuipitia walichoamua ni pamoja na kuwasimamisha viongozi wengine 16 na kufanya jumla ya viongozi waliosimamishwa na kuandikiwa barua za kujieleza hadi sasa kufika 23.
Mwakyembe alisema hatua ya kuwasimamisha wengine itaendelea itakapobainika nao wamefanya makosa.
Alisisitiza kuwa, lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha hadhi ya bandari inarejeshwa na kuboreshwa zaidi baada ya kubainika kuwepo kwa mapungufu mengi yaliyosababisha kupungua kwa ufanisi wa shughuli za mamlaka hiyo.
Waliosimamishwa ni Mkurugenzi wa Uhandisi, Mhandisi Mwandisi Bakari Kilo, Meneja Uhandisi, Mhandisi Raymond Swai, Ofisa Mhandisi Mkuu, Mary Mhayaya, Mkurugenzi wa Mipango, Florence Nkya, Meneja Ugavi na Ununuzi, Bahebe Machibya na Meneja Kitengo cha Ununuzi (PMU), Theophil Kimaro.
Wengine ni Mkurugenzi wa TEHAMA, Ayoub Kamti, Meneja Makasha, Mathew Anthony, Mkurugenzi wa Mifumo ya Menejimenti,
Dk Maimuna Mrisha, Meneja TEHAMA, Marcelina Mhando, Ofisa Ulinzi, Fortunatus Sandaria, Kitengo cha Marine Fadhili Ngorongo, KOJ Opereta Owen Rwebangira, Diver Mohamed Abdullah na Opereta Kilimba.
Aliyataja baadhi ya mapungufu yaliyobainika kwa mujibu wa taarifa hiyo ya uchunguzi kuwa ni kuwepo mgongano wa kimaslahi ambapo viongozi wa ndani ya mamlaka hiyo wamekuwa na kampuni zao ndogo ndogo zinazohudumia bandari.
“Huwezi kuendeleza mamlaka ya bandari kwa mtindo huu. Kama una maslahi yako huwezi kusimamia shughuli za mamlaka ipasavyo. Kama hiyo haitoshi tumekwenda hadi Brela hizo kampuni hazijasajiliwa, ni za mfukoni tu,” alisema.
Alisema wote waliobainika kuwa na kampuni hizo wameandikiwa barua wajieleze, kwa nini wasichukuliwe hatua za kisheria. Katika hatua nyingine Waziri Mwakyembe ametoa onyo kwa wale wote walioingia katika ajira kwa mipango bila sifa wajiondoe wenyewe kabla hawajafukuzwa kazi.
Alisema moja ya kikwazo cha ufanisi katika mamlaka hiyo ni ajira kutolewa bila kufuata taratibu na Sheria za Nchi na kuonya kuwa wale wanaojijua wameajiriwa kwa mtindo huo waache kazi wenyewe ili walipwe mafao yao badala ya kusubiri kuachishwa na kupoteza kila kitu.
Waziri Mwakyembe pia alizungumzia tatizo la kukithiri vitendo vya wizi ambavyo alivielezea kuwa na mtandao mkubwa. Hata hivyo, alisema tatizo hilo litakomeshwa kabisa.
“Haiwezekani kuruhusu hali hii iendelee. Inakuwaje kontena nzima inayeyuka kama kiberiti, huu ni mtandao mkubwa lazima tuukomeshe kabisa,“ alisema.
Alisema inatia aibu kuona mapato ya Bandari ya Dar es Salaam kwa mwezi ni Sh milioni 27 hadi 28 kwa mwezi wakati Mombasa ni Sh bilioni tatu. Hata hivyo alisema tangu mwezi Septemba ufanisi mzuri umekuwepo hadi mapato yameongezeka.
“Wale walizoea mchezo huu wa kuchuma kwa njia ya wizi nitawakamata, pamoja na wale wanaoiba vitu humu ndani na kufanya biashara ya kuuza kwa kushirikiana na wale deiwaka wanaosimama hovyo kwenye kijiwe nje, nitawakamata pia,” alisema.
Alipiga marufuku utaratibu wa kulipisha mawakala Sh 200 kama pasi ya bandari (port pass) na badala yake ametaka mamlaka
kuweka utaratibu wa kudhibiti watu kuingia hovyo na kuhakikisha kila mmoja ana kitambulisho kinachoeleweka na anajulikana
anakwenda wapi na anakwenda kufanya kitu gani.(CHANZO:HABARI LEO)

Friday, December 21, 2012

LEMA ASHINDA RUFAA YA UBUNGE

Mbunge Godbless Lema akiwahutubia wafuasi wake baada ya Hukumu.



DAR ES SALAAM-TANZANIA,Mahakama ya Rufani ya Jijini Dar es Salaam, imemrejea ubumbe, mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema (Chadema).    Lema alieyechaguliwa kuwa Mbunge kwa tiketi ya Chadema, katika uchaguzi mkuu uliopita, ubunge wake ulisita baada ya kuvuliwa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Aprili 15, mwaka huu, katika kesi ya kupinga ushindi wake iliyopelekwa mahakamani na baadhi ya wana-CCM.Kwa mujibu wa hukumu imeangalia haswa swala la Locus Stand ya kama waliofungua kesi walikuwa na haki kisheria ya kufanya hivyo.Hivyo kwa kina imeonekana kuwa kadiri ya pingamizi ya mawakili wa lema kimomogoro na Tundu Lissu,waliofungua shitaka dhidi ya lema hawakuwa na locus stand ya kufanya hivyo.kwa hiyo mengine yote yanakuwa null and void.Hukumu hiyo imechukua muda usiozidi nusu saa.kwa hiyo kwa taarifa hiyo Lema amerudi kuwa mbunge halali wa Arusha kuanzia leo.
Taarifa rasmi itaendelea kutolewa hapa Anga za Kimataifa kwa kadiri ya vyanzo vyetu.
(CHANZO:MJENGWA BLOG).

Wednesday, December 19, 2012

MAJAMBAZI WAPORA MILIONI 150 DAR.



Majeruhi wa tukio la ujambazi lililotokea Kariakoo, Dar es Salaam wakiwa kwenye gari la Polisi wakipelekwa hospitali baada ya kunusurika vifo wakati watu wanaodhaniwa kuwa majambazi walipowafyatulia risasi na kupora fedha kutoka kwa mhasibu wa duka la Artan Ltd jana. (Picha na Evance Ng’ingo).
DAR ES SALAAM-TANZANIA,
MAJAMBAZI waliokuwa wamepanda pikipiki kwa mtindo maarufu wa mshikaki, wamevamia duka la Kampuni ya Artan Ltd na kupora Sh milioni 150, zilizokuwa zikitolewa dukani eneo la Kariakoo kwenda benki jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa za Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, uporaji huo ulifanyika pamoja na mauaji jana saa 4:45 asubuhi katika Mtaa wa Mahiwa na Livingstone, Kariakoo. Kampuni hiyo inajihusisha na uuzaji wa betri na magurudumu.
Akisimulia mkasa huo jana, Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema majambazi hao waliwavamia watumishi wa kampuni hiyo waliokuwa wakitoa fedha katika duka lao kuzipeleka benki.
Alisema wakati wameshazi toa nje na kuingiza katika buti la gari aina ya Toyota Corolla Saloon ambayo haijafahamika namba, majambazi hao watatu wakiwa katika pikipiki yenye namba T301 CCW, mmoja akiendesha na wawili wakiwa wamepanda kwa mtindo wa mshikaki, waliwazingira huku wakiwaamuru watumishi hao kushuka katika gari ili waondoke nalo.
“Baada ya hao watumishi kukataa, majambazi hawa waliamua kuwajeruhi kwa risasi katika sehemu mbalimbali za miili yao na kufanikiwa kuondoka na fedha hizo,” alisema Kova.
Kati ya majeruhi hao kwa mujibu wa Kova, mmoja ni ambaye ni mhasibu wa kampuni hiyo, Ahmed Issa (55) alifariki dunia kutokana na kuumizwa vibaya na risasi hiyo.
Kova alisema mwingine aliyeuawa ni mwendesha mkokoteni, Sadik Juma (38) ambaye alinyanyua jiwe ili awapige majambazi hao waliokuwa katika pikipiki wakiondoka na fedha hizo, lakini kabla ya kurusha, walimuwahi na kumpiga risasi ya kichwa.
Majeruhi mwingine aliyekuwa katika gari lililomiminiwa risasi wakati wa uporaji wa fedha hizo, Yussuf Issa ambaye ni mtoto wa mwenye mali, anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Polisi waingilia kati
Kamanda Kova alisema mara baada ya kusikika kwa milio ya risasi, Polisi waliokuwa doria walifika eneo la tukio na kushirikiana na wananchi kuwasaka majambazi hao.
Alisema katika muda usiozidi robo saa, walimkamata mtuhumiwa wa kwanza aliyekimbilia kujificha katika Mtaa wa Kongo, Agustino Kayula ambaye kwa jina lingine anajulikana kama Frank Mwabinga (24).
“Huyu mtuhumiwa wa kwanza alikamatwa akiwa na bastola aina ya Browing ambayo ilikuwa imefutwa namba ikiwa na risasi moja na maganda matano ya risasi yalipatikana eneo la tukio na pikipiki hiyo,” alisema Kamanda Kova na kudai kuwa mtuhumiwa huyo amekiri kutumia silaha hiyo.
Kova alisema Polisi pia inamshikilia mlinzi wa duka hilo, Ally Said (42) kwa tuhuma za kula njama ili kufanikisha uporaji huo kutokana na kushindwa kupambana na majambazi hao licha ya kuwa na silaha. Mlinzi huo amedai kuwa bunduki yake haipigi risasi.
“Huyu mlinzi inaonekana kuna namna fulani amefanya maana alidai kuwa bunduki yake haipigi risasi, lakini tumeikagua ni nzima kabisa na inafanya kazi, licha ya hivyo majambazi waliwezaje kumuacha mtu ambaye ana silaha na kuwafuata watu wale moja kwa moja?” Alihoji Kova.
Muuza maji ndani
Kova alisema Polisi pia inawashikilia watuhumiwa wengine wawili mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Mussa maarufu Alhaji, anayesukuma mkokoteni na Salum Athumani, muuza maji ambao waliletwa kwa msaada wa wananchi wakiwa wamejeruhiwa.
Alisema pamoja na kuwashikilia watu hao, lakini hawezi kuwaunganisha moja kwa moja mpaka uchunguzi utakapokamilika.
Maziko ya Sadik
Kamanda Kova alisema Sadik aliyeuawa wakati akijaribu kuwapiga jiwe majambazi hao, alikuwa akisaidia Polisi na kutokana na mchango wake, wanaahidi kushirikiana na familia kuhakikisha maziko yanafanyika salama.
Pia amewaonya wahalifu kuwa katika kuelekea Sikukuu za mwisho wa Mwaka mpya, polisi wamejipanga vizuri na wanaendelea na msako mkali.(CHANZO:HABARI LEO)

KESI YA MAUAJI YA KANUMBA-LULU ABADILISHIWA MASHITAKA




DAR ES SALAAM-TANZANIA,
Upande wa mashtaka hapo ulimbadilishia mashitaka msanii Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu kutoka kuua kwa kukusudia hadi kuua kwa kutokukusudia katika tuhuma za kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba.Kwa  mabadiliko hayo Lulu ameepuka adhabu ya kunyongwa hadi kufa.  baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kumbadilishia mashtaka, ambapo sasa anatuhumiwa kuua bila kukusudia, ingawa kama atapatikana na hatia , adhabu yake ni kifungo cha maisha au hata  kuachiwa huru.

Hii inatokana na kifungu cha 196 cha kanuni za adhabu ya kosa la kuua bila kukusudia, ambapo anayepatikana na hatia anaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha, miaka kadhaa au kuachiwa huru.

Hata hivyo, baadhi ya wanasheria waliliambia gazeti hili kwamba uzoefu wa adhabu nyingi za kuua pasipo kukusudia zilizowahi kutolewa nchini, ni kati ya miaka 15 na wengine waliachiwa huru.

Lulu alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Aprili 11, mwaka huu akikabiliwa na tuhuma za kumuua Kanumba Aprili 7, 2012.

Alikuwa akidaiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 196 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), shtaka ambalo mshtakiwa anayepatikana na hatia adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa.

Hata hivyo, jana upande wa mashtaka ulieleza mahakamani kuwa kwa sasa imebadilisha mashtaka kutoka kuua kwa kukusudia na kuwa kuua bila kukusudia, kinyume cha kifungu cha 195 cha CP.

Mshtakiwa huyo alitarajiwa kusomewa mashtaka hayo mapya jana pamoja na maelezo yote ya kesi, ambapo angesomewa ushahidi wa mashahidi wote pamoja na vielelezo muhimu katika kesi hiyo.

Hata hivyo, hatua hiyo ilikwama kutokana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka anayeiendesha kesi hiyo kutokuwapo mahakamani na badala yake aliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Ofmedy Mtenga.

“Upelelezi wa shauri lako umeshakamilika na tungeweza kukusomea comital (maelezo ya kesi) leo, lakini kwa kuwa waendesha mashtaka hawapo basi tunaliahirisha mpaka tarehe nyingine.”, alisema Hakimu Mkazi Agustina Mmbando, anayesikiliza kesi hiyo katika hatua hiyo ya awali.

Taarifa hizo za kukamilika kwa ushahidi wa kesi hiyo zilipokewa kwa furaha na shangwe na msanii huyo, kiasi kwamba alishindwa kujizuia kuonyesha furaha yake.

Wakili wake Peter Kibatala aliiomba mahakama itoe ahirisho fupi hadi Ijumaa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa mashtaka haya mapya pamoja na maelezo ya awali.
Hakimu Mmbando alikubaliana na ombi hilo la Wakili Kibatala na akaahirisha kesi hiyo hadi Ijumaa.(CHANZO:MWANANCHI)

Tuesday, December 18, 2012

SIRI ZAIDI ZAFICHUKA MAUAJI YA POLISI NA RAIA KAGERA.

KAGERA-TANZANIA,
Mambo Mapya yameendelea kuibuka kufuatia madai kuwa vifo vya watu watatu wakiwamo polisi wawili wilayani Ngara mkoani Kagera vimetokana na askari hao kukusanya kwa nguvu mapato ya serikali.



Chanzo chetu kimeeleza kuwa Askari wa Usalama Barabarani wanapaswa kukusanya kiasi kisichopungua Shilingi milioni tatu kila mwezi na hatua hiyo imekuwa ikiwalazimu kwenda kukamata na kutoza faini mbalimbali katika maeneo hata yasiyo na usalama kwa maisha yao.

Kikizungumzia tukio la mauaji hayo, chanzo hicho kilidai kuwa kitendo cha polisi kwenda kukamata pikipiki iliyokuwa ikitengenezwa na mtuhumiwa huyo ambaye ni fundi jirani na gulio la kijiji hicho, hakikuzingatia taratibu.



Kwa msingi huo, chanzo hicho kimeeleza kwamba Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani ndiye anayepaswa kuwa mlalamikiwa wa kwanza katika mauaji hayo.

“Unajua ndugu mwandishi, haiwezekani kwenda kukamata pikipiki za watu hadi ndani ya gulio...mbaya zaidi unakwenda kukamata na pikipiki inayotengenezwa kwa fundi. Hakika hapa busara haikutumika hata kidogo, ndiyo maana mauaji kama haya yametokea,” kilidai chanzo hicho na kuongeza:
“Pamoja na kwamba Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani kuwa mlalamikiwa wa kwanza, kwa kiasi kikubwa serikali yetu nayo inachangia maana sisi askari wa usalama barabarani tunalazimika kuhakikisha tunafikisha kiwango cha fedha tunazopangiwa kwa kila mwezi na inapotokea tarehe zinaelekea ukingoni na makusanyo hayajafikia, matokeo yake ndiyo hayo.” 
Chanzo hicho kilipingana na taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi, kwamba askari hao walikuwa kwenye operesheni maalum ya kukamata watu wasio na leseni na vyombo vya moto visivyofaa kwa matumizi ya usafirishaji wa abiria.




Kwa mujibu wa chanzo hicho, taarifa hiyo imechakachuliwa kwa lengo la kukwepesha ukweli wa jambo hilo kujulikana.

“Hakika hapakuwa na operesheni maalum kama Kamanda alivyodai isipokuwa ni utaratibu wetu wa kawaida kwenda kukusanya mapato ya serikali. Tatizo hapa ni kutaka kukwepesha ukweli wa mambo. Aidha, yeye mwenyewe au mkuu wa upelelezi wa wilaya ambaye atakuwa ameamua kuchakachua maelezo ili kuweka kinga ya kuonekana askari walikuwa kwenye makosa,” kilidai chanzo hicho.



Hata hivyo, Kamanda Kalangi alipoulizwa jana kuhusiana na taarifa hiyo, alisisitiza kuwa ilikuwa operesheni.

“Mimi ndiye Kamanda, kama kuna anyepinga taarifa nilizozitoa kamuulize huyo huyo,” alisema Kamanda Kalangi.



Alisema kutokana na mauaji hayo, Mkuu wa Polisi nchini, Said Mwema, ametuma kikosi maalum kutoka makao makuu ya polisi kinachotarajiwa kuingia mkoani Kagera jana. Hata hivyo, hadi jioni hakikuwa kimewasili. 

Alisema kikosi hicho kitaungana na wenzao wa mkoani Kagera kuchunguza kwa kina mauaji hayo askari hao wawili pamoja na raia mmoja.

Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zimedai kuwa askari hao wa Kikosi cha Usalama Barabarani, walikwenda katika kijiji na kata ya Mugoma kukamata vyombo vya usafiri na watu wanaoendesha bila leseni ili kuhakikisha wanafikisha kiwango cha makusanyo ya serikali waliyopangiwa kila mwezi.(CHANZO:IPP MEDIA)

JACOB ZUMA ASHINDA TENA UCHAGUZI ANC.


Jacob Zuma
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amechaguliwa tena kuongoza chama tawala nchini humo cha ANC baada ya kupata kura 2.983 dhidi ya 3.977 ya kura zilizopigwa, ikiwa ni ishara ya kumfagilia njia ya kuelekea kwenye uchanguzi wa rais mwaka 2014.

Makamu wa rais wa Afrika Kusini Kgalema Motlenthe ambae awali alitangaza kuwania nafasi hiyo ameonekana kuanguka kisiasa baada ya kuchukuwa uamuzi huo na mwishowekujiondowa ili aendelee kukalia kwenye nafasi yake, ambayo sasa ameikosa.
Cyril Ramaphosa, mfanyabiashara maharufu nchini humo amechukuwa nafasi ya makamu mwenyekiti wa chama, na kumrithi Motlanthe. Cyril Ramaphosa, ni mtu wa karibu sana na rais Zuma na huenda akawa mrithi wa zuma katika chaguzi zijazo, iwapo Jacob Zuma ataamua kutowania muhula mwingine
Zuma alipewa nafasi ya kushinda uchaguzi huo, licha ya kukabiliwa na kashfa mbalimbali na suala la kukigawa chama hicho, kwani asilimia kubwa ya wajumbe wakuu wa chama hicho wanamuunga mkono.
Akiwahutubia wajumbe hao zaidi ya elfu nne siku ya jumapili iliopita, Jacob Zuma aliahidi kupiga vita suala la kukigawa chama na rushwa inayo kithiri ambapo mwenye amehusishwa kutumia vibaya mali ya umma kwa manufaa yake binafsi.
Mbali na hayo Zuma aliahidi pia kupambana na hali ya mgawanyiko katika chama na mzozo uliotikisa nchi hiyo kufuatia mgomo wa wafanyakazi wa migodini uliopelekea watu zaidi ya sitini kupoteza maisha.
Jacob Zuma ametetea utawala wake huku akiahidi kuboresha zaidi na kutia kipao mbele masuala ya elimu, kuopiga vita rushwa na kupiga vita wawindaji haramu wa mifugo ya vifaru.
Wajumbe wa chama cha ANC walianza kukutana tangu siku ya Jumapili iliopita huko Bloenfontein na kutamatisha kikao hicho baada ya kuwapata viongozi hao wapya.(CHANZO:RFI)

Monday, December 17, 2012

OBAMA AWAFARIJI WAOMBOLEZAJI WA MAUAJI MAREKANI


US-Präsident Barack Obama spricht auf der Trauerfeier für die Opfer des Amoklaufs von Newtown (Foto: dpa)Rais wa Marekani Barack Obama ameahidi kutumia mamlaka yake yote kuhakikisha kuwa mikasa ya mauwaji yanayotokana na mashambulizi ya kiholela ya risasi haitokei tena.
Akizungumza katika mkesha wa maombolezii mjini Newtown ya watu 26 waliouawa katika shule moja ya msingi wakiwemo watoto 20, Obama amesema Marekani haifanyi vya kutosha katika kuwalinda watoto wake, na akaahidi kwamba katika wiki zijazo, ataanzisha juhudi za kupunguza mashambulizi kama hayo nchini humo.
Lazima kufanywe mabadiliko
Biwi la simanzi bado limetanda katika mji wa Newtown, ConnecticutBiwi la simanzi bado limetanda katika mji wa Newtown, Connecticut
Rais Obama amesema matukio ya mauwaji ya mashambulizi ya risasi hayawezi tena kuvumiliwa na ni lazima yafikie kikomo. Na kwa kutimiliza hilo, ni lazima pawepo mabadiliko. Rais huyo wa Marekani ameeleza mapenzi yake na maombi ya taifa kwa jumla kwa familia za wahanga wa mauwaji hayo, akisema Wamarekani wote wanasimama pamoja nao katika kuomboleza vifo hivi vya kikatili. Rais Obama ametoa wito wa dharura kwa Wamarekani kufanya kila wawezalo kuzuia kutokea tena mikasa isiyo na idadi ya ufyatuwaji risasi ambayo imeitia hofu nchi hiyo. Tangu kuchaguliwa kuwa rais, Obama ameshuhudia matukio manne makuu ya mauwaji ya kiholela kupitia risasi, lakini kumekuwa na visa vingine vidogo vilivyotokea katikati ya matukio hayo.
Hakuna sheria inayoweza kuangamiza maovu duniani
Obama amekiri kwamba hakuna sheria yoyote inayoweza kutokomeza uovu duniani au kuzuia kila aina ya mauwaji katika jamii, lakini akadokeza kwamba atatafuta ufumbuzi wa suala hilo. Awali, maafisa walimtambua rasmi Adam Lanza, mwenye umri wa miaka 20, kuwa ndiye aliyefanya shambulizi hilo, wakithibitisha kwamba alimpiga risasi mamake mara kadhaa kichwani katika nyumba walimoishi, kabla ya kuelekea katika shule hiyo yake ya zamani na kufanya kitendo hicho cha kinyama.
Mamia wamehudhuria mkesha wa maombi ya wahanga wa mauwajiMamia wamehudhuria mkesha wa maombi ya wahanga wa mauwaji
Polisi imesema Lanza alitumia bunduki ya mamake aina ya bushmaster 223 kuwauwa watu 26 shuleni humo, ikiwa ni pamoja na watoto 20 wenye kati ya umri wa miaka sita na saba, kabla ya kujiuwa na bastola wakati polisi walipowasili shuleni humo huku ving'ora vya magari vikilia.
Waombolezaji waliohudhuria ibada hiyo iliyofanyika katika shule ambako kulitokea mkasa huo ya Sandy Hook, wametiririkwa na machozi wakati rais alipokuwa akiyasoma majina ya kila mmoja aliyeuawa katika shambulizi hilo siku ya Ijumaa. Mazishi ya wawili kati ya watoto 20 waliouawa katika mkasa huo yatafanywa leo. Wakati huo huo, shule kote Marekani zinafunguliwa tena hii leo huku watoto waliojawa hofu wakijiuliza ni kwa nini wenzao wakauliwa kinyama katika jimbo la Connecticut, na kama wako salama dhidi ya tukio jingine kama hilo
Mauwaji yazusha mjadala
Mauaji hayo yameamsha upya mjadala juu ya udhibiti wa silaha katika nchi ambapo utamaduni wa kumiliki silaha umeshamiri na kuna ushawishi mkuwa wa kupigia debe umilikaji wa silaha, jambo ambalo limewakatisha tamaa wanasiasa wengi kufanya jitihada zozote zile kubwa za kushughulikia tatizo la kumiliki silaha kwa urahisi. Meya wa mji wa New York Michael Bloomberg ambaye anaongoza muungano wa mameya katika suala la sera ya silaha amesema hapo Ijumaa kwamba Rais Obama wa chama cha Demokrat anapaswa kuchukuwa hatua licha ya upinzani kutoka chama cha Republikan ambacho kinalidhibiti Baraza la Wawakilishi la bunge la Marekani. Bloomberg amesema katika taarifa " Tumeyasikia madoido ya kusema kabla.Hatukushuhudia uongozi sio kutoka Ikulu wala kutoka bungeni. Jambo hilo halina budi kukomeshwa leo hii."( CHANZO: DW)

FAINALI YA KLABU BINGWA ZA DUNIA: CHELSEA YASHINDWA KWA COLITHIANS.


Klabu ya Corrinthians kutoka Brazil, imeshinda kombe la klabu bingwa duniani baada ya kuilaza Chelsea bao moja kwa bila katika mechi ya fainali iliyochezwa nchini Japan.
Paolo Guerrero aliifungia Corinthians, bao hilo muhimu na la ushindi.
Hata hivyo Chelsea, ilipoteza bafasi nyingi za kufunga wakati wa mechi hiyo.
Katika muda wa ziada Fernando Torres, alipoteza nafasi nzuri sana ya kuzawazisa licha ya kuwapiku walinzi wa Corinthians na kubakia kipa pekee.
Torres alijaribu kumchenga kipa wa Corinthians lakini kombora lake likawa hafifu na kudakwa kwa urahisi na kipa.
Chelsea ilimaliza mechi hiyo ikiwa na wachezaji kumi baada ya Gary Cahil, kupewa kadi nyekundu baada ya kumfanyika madhambi mchezaji wa Corrinthians Emerson.
Bao la chelsea lililofuingwa kwa kichwa na Fernando torres lilikataliwa na hivyo vijana hao kutoka brazil wakaibuka na ushindi.( CHANZO:BBC)

Sunday, December 16, 2012

WANANCHI WAUA POLISI WAWILI KAGERA


KAGERA-TANZANIA,
WANANCHI wa Kata ya Mugoma, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera wamewaua askari polisi wawili na kuchoma moto Kituo cha Polisi Mugoma kwa madai kuwa polisi hao wamemuua kwa kumpiga risasi mwananchi mwenzao bila hatia.
Tukio hilo la lilitokea jana mchana wilayani humo na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi.
Akizungumza wakati akielekea eneo la tukio, Kamanda Kalangi alisema: “Tukio limetokea Kijiji cha Mugoma, sina details (maelezo ya kina), kwa sababu ndiyo nakwenda huko, ila nikifika ndipo nitajua nini kimetokea, nitatoa maelezo kwa kina.”
Habari zilizorushwa na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC), jana jioni zilieleza kuwa askari polisi waliouawa ni Koplo Pascal na Konstebo Alex wa Kikosi cha Usalama Barabarani wilayani Ngara.
Katika taarifa hiyo ya BBC, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Costa Kanyasu naye alithibitisha vifo vya askari hao na kueleza kuwa wanaendelea kufanya uchunguzi kujua ukweli wa tukio hilo, ikiwa ni pamoja na kujua kama askari hao ndiyo walimpiga risasi mwananchi huyo.
Ilidaiwa kuwa polisi hao walifika katika Kijiji cha Mugoma kwa lengo la kukagua pikipiki mbovu na zisizokuwa na usajili.
Walipokuwa katika ukaguzi huo walifika katika gereji moja na kukuta mmiliki wake akitengeneza pikipiki, wakamtaka aipeleke kituoni kwa maelezo kuwa ilikuwa mbovu.
Ilidaiwa kuwa fundi huyo aligoma kutekeleza amri hiyo na katika ubishi, polisi mmoja alimpiga risasi na kufariki dunia papohapo.
Kitendo hicho kiliamsha hasira kwa wananchi waliokuwa jirani na eneo hilo ambao walianza kujikusanya katika eneo la tukio.
Mmoja wa watu mashuhuda wa tukio hilo, Mwandishi wa Habari wa Redio Kwizera iliyopo wilayani Ngara, Joyce Ngalawa alisema kuona hivyo, polisi anayedaiwa kufyatua risasi alikimbia na kujificha katika nyumba iliyopo jirani na gereji hiyo, huku akimwacha mwenzake.
“Wananchi walimvamia yule askari aliyebaki pale gereji na kuanza kumkata kwa mapanga na kumpiga mawe hadi akafariki dunia,” alisema.
Alisema baada ya mauaji hayo, wananchi hao walikwenda katika nyumba aliyokuwa amejificha askari wa pili na kutishia kuichoma moto iwapo angegoma kutoka.
“Mmiliki wa nyumba ile baada ya kuona wananchi hao wanataka kuichoma moto nyumba yake, alimtaka askari huyo atoke nje. Alipotoka tu, wananchi walimvamia na kuanza kumpiga mawe na kumuua,” alisema.(CHANZO:MWANANCHI)

Saturday, December 15, 2012

TYSON AKANUSHA KUBADILI JINSIA



"I have no intention of becoming a woman": Mike Tyson sex change spoof fools African media

Spoof story reported "Iron Mike" had undergone a 16-hour sex change operation and changed his name to Michelle, the "Iron Maiden"
Iron Mike: In his prime Tyson was dubbed "The Baddest Man on the Planet"

MAREKANI,

Bingwa zamani wa uzito wa juu Mike  'Iron' Tyson amekanusha vikali taarifa zilizoenea katika mitandao ya kiafrika wiki hii zikiunuku mtandao wa NewsBiscuit  wa Uingereza kuwa amebadili jinsia pamoja na jina na kuitwa Michelle.

Katika taarifa yake hiyo Tyson amesema hajabadilisha jinsia yake na wala hana mpango wa kufanya hivyo na taarifa hizo siyo tu za kushangaza bali za zisizo na maana yoyote.


Ndani ya wiki hii mitandao mingi ya kiafrika ikiwepo wavuti yetu ya Anga za kimataifa ilichapisha taarifa hiyo ikiunukuu mtandao wa The Standard wa Zimbamwe na NewsBiscuit wa Uingereza. Hivyo kwa taarifa hizo rasmi tunakanusha taarifa hiyo na kuomba radhi kwa wasomaji wetu kwa usumbufu wowote uliojitokeza tukiahiddi kuhakiki ukweli wa habari na vyanzo vyetu kwa wakati ujao.


MAREKANI KUTUMA MAKOMBORA UTURUKI



WASHINGTON-MAREKANI, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Leon Panneta ameagiza kutumwa kwa makombora  katika mpaka wa Uturuki na Syria pamoja na wanajeshi 400 kuilinda Uturuki dhidi ya uvamizi wa kijeshi kutoka  Syria.

Hatua hiyo pia imeungwa mkono na muungano wa majeshi ya Mataifa ya Magharibi NATO, baada ya Uturuki kuomba msaada huo ili kujilinda.

Panneta amesema makombora hayo yanatarajiwa kuwekwa katika mpaka huo katika siku chache zijazo ili kuisadia Uturuki ambayo ni washirika wake wa karibu.
Mataifa ya Ujerumani na Uholanzi pia yamekubali kuleta makombora yake ili kuisaidia Uturuki katika uvamizi wowote kutoka Syria.
Hii inakuja siku chache baada ya wasiwasi kuzuka kuwa serikali ya Syria inapanga kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia wake na pia kulenga jirani zao Uturuki ambao wameendelea kushinikiza kujiuzulu kwa rais Bashar Al Assad.
Kwingineko,Urusi imekanusha habari zilizotolewa siku ya Alhamisi na Naibu Waziri wa Mambo ya nje Mikhail Bogdanov kuwa waasi wanaelekea kuwashinda wanajeshi wa serikali.
Wizara ya mambo ya nje nchini humo imesisitiza kuwa matamshi ya Bogdanov hayakumaanisha kuwa sera na msimamo wa Urusi imebadilika kuhusu rais Bashar Al Assad ambaye wataendelea kumuunga mkono.
Marekani ilikuwa imepongeza mtazamo huo wa Urusi kwa kile walichokisema kuwa nchi hiyo ilikuwa sasa inatambua kinachoendelea nchini humo na kuanza kubadilisha msimao wake.

Mapigano kati ya wapiganaji wa upinzani na majeshi ya serikali ya Syria yameingia katika mwaka wake wa pili na kusababisha zaidi ya vifo vya watu elfu 40.(CHANZO:RFI)