Wednesday, December 5, 2012

KUELEKEA UCHAGUZI KENYA-Mudavadi ajiunga kambi ya Ruto na Uhuru, huku Odinga, Musyoka, Wetangula na Ngilu waunda kambi yao



Waziri mkuu Raila Odinga na makamu wa rais Kalonzo Musyoka wakitia saini muungano wa vyama vyao vya ODM/WIPER/FORD-K/NARC
Waziri mkuu Raila Odinga na makamu wa rais Kalonzo Musyoka wakitia saini muungano wa vyama vyao vya ODM/WIPER/FORD-K/NARC
RFI
















NAIROBI-KENYA, Harakati za kisiasa nchini Kenya zimeendelea kushika hatamu kufuatia wagombea mbalimbali wanaowania urais kutangaza miungano yao na vyama vingine kwa lengo la kuhakikisha wanapata ushindi kwenye uchaguzi mkuu wa hapo mwakani.

Muungano wa kwanza ulikuwa ni ule wa vyama vya URP cha mbunge wa Eldoret kaskazini William Ruto na mwenzake wa TNA ambaye pia ni naibu waziri mkuu Uhuru Kenyatta kutiliana saini siku ya Jumapili.
Tarahe 4 ya mwezi huu ndio ilikuwa siku ya mwisho kwa vyama mbalimbali kutangaza miungano yao ambapo waziri mkuu Raila Odinga na chama chake cha ODM kilitangaza kuungana na chama cha Wiper cha makamu wa rais Kalonzo Musyoka na kile cha FORD-K cha Moses Wetangula.
Kuungana kwa waziri mkuu raila Odinga na makamu wa rais Kalonzo Musyoka kulitabiriwa na wachambuzi wa masuala ya siasa ambao walisema kutokana na viongozi hao kuungana mwaka 2002 chini ya mwavuli wa NARC kulikuwa na uwezekano mkubwa pia kwa mwaka huu kuungana kwaajili ya uchaguzi ujao na sasa watakuwa chini ya mwavuli wa CORD.
Katika muungano wao mbali na kuwepo kwa chama cha FORD-K Moses Wetangula, pia mwenyekiti wa chama cha NARC Charity Ngilu alitangaza kujiunga kwenye muungano huo ambao sasa unajumuisha vyam 14.
Viongozi wote kwa pamoja wameapa kuwaunganisha wakenya na kuijenga kenya bora isiyo na migogoro ya kidini wala kikabila kama ilivyojitokeza kwenye uchaguzi wa mwaka 2007/2008.
Katika hatua nyingine naibu waziri mkuu Musalia Mudavadi wa chama cha UDF alitangaza kuungana na William Ruto na Uhuru Kenyatta katika mbio za kuwania kuingia ikulu mwaka 2013.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaona kuwa licha ya kuwepo miungano ya vyama mbalimbali bado viongozi hao wanachangamoto kubwa ya kuhakikisha wanaondoa ukabila ambao baadhi ya wagombea wametuhumiwa kujiunga kutokana na maeneo wanayotoka.
Muungano wa CORD kati ya Raila Odinga na Kalonzo Musyoka bado wenyewe hawajatangaza ni nani atakayewania kiti cha urais na jambo hilo litaamuliwa kwenye mkutano mkuu wa vyama vyao.(CHANZO RFI)

No comments:

Post a Comment