Wednesday, December 19, 2012

MAJAMBAZI WAPORA MILIONI 150 DAR.



Majeruhi wa tukio la ujambazi lililotokea Kariakoo, Dar es Salaam wakiwa kwenye gari la Polisi wakipelekwa hospitali baada ya kunusurika vifo wakati watu wanaodhaniwa kuwa majambazi walipowafyatulia risasi na kupora fedha kutoka kwa mhasibu wa duka la Artan Ltd jana. (Picha na Evance Ng’ingo).
DAR ES SALAAM-TANZANIA,
MAJAMBAZI waliokuwa wamepanda pikipiki kwa mtindo maarufu wa mshikaki, wamevamia duka la Kampuni ya Artan Ltd na kupora Sh milioni 150, zilizokuwa zikitolewa dukani eneo la Kariakoo kwenda benki jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa za Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, uporaji huo ulifanyika pamoja na mauaji jana saa 4:45 asubuhi katika Mtaa wa Mahiwa na Livingstone, Kariakoo. Kampuni hiyo inajihusisha na uuzaji wa betri na magurudumu.
Akisimulia mkasa huo jana, Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema majambazi hao waliwavamia watumishi wa kampuni hiyo waliokuwa wakitoa fedha katika duka lao kuzipeleka benki.
Alisema wakati wameshazi toa nje na kuingiza katika buti la gari aina ya Toyota Corolla Saloon ambayo haijafahamika namba, majambazi hao watatu wakiwa katika pikipiki yenye namba T301 CCW, mmoja akiendesha na wawili wakiwa wamepanda kwa mtindo wa mshikaki, waliwazingira huku wakiwaamuru watumishi hao kushuka katika gari ili waondoke nalo.
“Baada ya hao watumishi kukataa, majambazi hawa waliamua kuwajeruhi kwa risasi katika sehemu mbalimbali za miili yao na kufanikiwa kuondoka na fedha hizo,” alisema Kova.
Kati ya majeruhi hao kwa mujibu wa Kova, mmoja ni ambaye ni mhasibu wa kampuni hiyo, Ahmed Issa (55) alifariki dunia kutokana na kuumizwa vibaya na risasi hiyo.
Kova alisema mwingine aliyeuawa ni mwendesha mkokoteni, Sadik Juma (38) ambaye alinyanyua jiwe ili awapige majambazi hao waliokuwa katika pikipiki wakiondoka na fedha hizo, lakini kabla ya kurusha, walimuwahi na kumpiga risasi ya kichwa.
Majeruhi mwingine aliyekuwa katika gari lililomiminiwa risasi wakati wa uporaji wa fedha hizo, Yussuf Issa ambaye ni mtoto wa mwenye mali, anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Polisi waingilia kati
Kamanda Kova alisema mara baada ya kusikika kwa milio ya risasi, Polisi waliokuwa doria walifika eneo la tukio na kushirikiana na wananchi kuwasaka majambazi hao.
Alisema katika muda usiozidi robo saa, walimkamata mtuhumiwa wa kwanza aliyekimbilia kujificha katika Mtaa wa Kongo, Agustino Kayula ambaye kwa jina lingine anajulikana kama Frank Mwabinga (24).
“Huyu mtuhumiwa wa kwanza alikamatwa akiwa na bastola aina ya Browing ambayo ilikuwa imefutwa namba ikiwa na risasi moja na maganda matano ya risasi yalipatikana eneo la tukio na pikipiki hiyo,” alisema Kamanda Kova na kudai kuwa mtuhumiwa huyo amekiri kutumia silaha hiyo.
Kova alisema Polisi pia inamshikilia mlinzi wa duka hilo, Ally Said (42) kwa tuhuma za kula njama ili kufanikisha uporaji huo kutokana na kushindwa kupambana na majambazi hao licha ya kuwa na silaha. Mlinzi huo amedai kuwa bunduki yake haipigi risasi.
“Huyu mlinzi inaonekana kuna namna fulani amefanya maana alidai kuwa bunduki yake haipigi risasi, lakini tumeikagua ni nzima kabisa na inafanya kazi, licha ya hivyo majambazi waliwezaje kumuacha mtu ambaye ana silaha na kuwafuata watu wale moja kwa moja?” Alihoji Kova.
Muuza maji ndani
Kova alisema Polisi pia inawashikilia watuhumiwa wengine wawili mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Mussa maarufu Alhaji, anayesukuma mkokoteni na Salum Athumani, muuza maji ambao waliletwa kwa msaada wa wananchi wakiwa wamejeruhiwa.
Alisema pamoja na kuwashikilia watu hao, lakini hawezi kuwaunganisha moja kwa moja mpaka uchunguzi utakapokamilika.
Maziko ya Sadik
Kamanda Kova alisema Sadik aliyeuawa wakati akijaribu kuwapiga jiwe majambazi hao, alikuwa akisaidia Polisi na kutokana na mchango wake, wanaahidi kushirikiana na familia kuhakikisha maziko yanafanyika salama.
Pia amewaonya wahalifu kuwa katika kuelekea Sikukuu za mwisho wa Mwaka mpya, polisi wamejipanga vizuri na wanaendelea na msako mkali.(CHANZO:HABARI LEO)

No comments:

Post a Comment