DAR ES SALAAM-TANZANIA,
NAHODHA aliyeiwezesha Timu ya Taifa ya Zambia (Chipolopolo) kuandika historia ya kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka huu, Christopher Katongo leo anakiongoza kikosi hicho katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Timu ya Taifa (Taifa Stars) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katongo, mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka BBC mwaka huu, atakikabili kikosi cha Stars katika mechi hiyo ya kihistoria na pekee kwa aina yake kwa timu hizo mbili.
Hii ni mara kwa kwanza kwa Zambia inayoshika nafasi ya 34 kwa viwango vya ubora katika Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kucheza na Stars inayoshika nafasi ya 130, kama bingwa mtetezi wa mataifa ya Afrika.
Hata hivyo, mara ya mwisho kabla ya mchezo wa leo, zilikutana mwaka jana wakati wa michuano ya Kombe la Chalenji kwenye Uwanja wa Taifa, shukrani kwa bao la Felix Sunzu lililoipa ushindi wa bao 1-0 Zambia dhidi ya Stars.
Chipolopolo ilitwaa taji la Afrika baada ya kuifunga timu iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa kutokana na kuundwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa sehemu mbambali duniani, Ivory Coast.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Chipolopolo Patrice Beaunelle alisema haifahamu vizuri Tanzania kwa miaka ya karibuni, na kwa sababu hiyo anatarajia mchezo huo utakuwa mgumu na upinzani mkali.
Beaunelle alisema kwa vile, haifahamu vizuri Stars inayofundishwa na Kocha Kim Poulsem, atakipanga kikosi chake kamili wakiwamo baadhi ya chipukizi walioonyesha kiwango kinachovutia.
Mbali na Katongo, wengine watakaoshuka dimbani kuivaa Stars ni
Felix Katongo,Isaac Chansa, Francis Kasonde na Given Singuluma.
Pia anatarajia kuwasili wachezaji wengine waliochelewa kujiunga na wenzao, ambao ni Stophira Sunzu na Rainford Kalaba.
Kwa upande wake Kocha Poulsen atakayeshusha kikosi kitakachowakosa wachezaji wa kulipwa, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu amesema mchezo utakuwa mgumu kwa vile wanakutana na timu yenye uwezo mkubwa.
Pia hatakuwa na mshambuliaji wake nyota, John Bocco aliyeumia wakati wa mazoezi, kama ilivyo kwa Samata na Ulimwengu ambao tangu kuwasili wameshindwa kufanya mazoezi na wenzao kwa sababu ya kuwa majeruhi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Poulsen alisema pamoja na kukosekana kwa wachezaji hao bado ana matumaini ya kuisimamisha Zambia inayojiandaa kwenda kutetea taji lao nchini Afrika Kusini mwezi ujao.
"Naipongeza Zambia kwa kukubali kuja nchini kucheza mechi ya kirafiki, tuna kila sababu ya kujivunia lakini hilo halitatufanya tucheze kwa kuiogopa," alisema Poulsen.
"Natumaini mechi hii itatusaidia kujifunza mengi na pia itakuwa ni kipimo kizuri kwa timu yetu kwa ajili ya mechi mbalimbali zilizopo mbele yetu za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia pamoja na zile za mashindano ya CHAN.
"Nawaomba Watanzania wajitokeza kwa wingi na kutuunga mkono katika mchezo huu na kukosekana kwa Samata, Ulimwengu na Bocco isiwe sababu ya kutokutuunga mkono," alisema Poulsen.(CHANZO:MWANANCHI)
No comments:
Post a Comment