Wednesday, December 19, 2012

KESI YA MAUAJI YA KANUMBA-LULU ABADILISHIWA MASHITAKA




DAR ES SALAAM-TANZANIA,
Upande wa mashtaka hapo ulimbadilishia mashitaka msanii Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu kutoka kuua kwa kukusudia hadi kuua kwa kutokukusudia katika tuhuma za kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba.Kwa  mabadiliko hayo Lulu ameepuka adhabu ya kunyongwa hadi kufa.  baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kumbadilishia mashtaka, ambapo sasa anatuhumiwa kuua bila kukusudia, ingawa kama atapatikana na hatia , adhabu yake ni kifungo cha maisha au hata  kuachiwa huru.

Hii inatokana na kifungu cha 196 cha kanuni za adhabu ya kosa la kuua bila kukusudia, ambapo anayepatikana na hatia anaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha, miaka kadhaa au kuachiwa huru.

Hata hivyo, baadhi ya wanasheria waliliambia gazeti hili kwamba uzoefu wa adhabu nyingi za kuua pasipo kukusudia zilizowahi kutolewa nchini, ni kati ya miaka 15 na wengine waliachiwa huru.

Lulu alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Aprili 11, mwaka huu akikabiliwa na tuhuma za kumuua Kanumba Aprili 7, 2012.

Alikuwa akidaiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 196 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), shtaka ambalo mshtakiwa anayepatikana na hatia adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa.

Hata hivyo, jana upande wa mashtaka ulieleza mahakamani kuwa kwa sasa imebadilisha mashtaka kutoka kuua kwa kukusudia na kuwa kuua bila kukusudia, kinyume cha kifungu cha 195 cha CP.

Mshtakiwa huyo alitarajiwa kusomewa mashtaka hayo mapya jana pamoja na maelezo yote ya kesi, ambapo angesomewa ushahidi wa mashahidi wote pamoja na vielelezo muhimu katika kesi hiyo.

Hata hivyo, hatua hiyo ilikwama kutokana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka anayeiendesha kesi hiyo kutokuwapo mahakamani na badala yake aliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Ofmedy Mtenga.

“Upelelezi wa shauri lako umeshakamilika na tungeweza kukusomea comital (maelezo ya kesi) leo, lakini kwa kuwa waendesha mashtaka hawapo basi tunaliahirisha mpaka tarehe nyingine.”, alisema Hakimu Mkazi Agustina Mmbando, anayesikiliza kesi hiyo katika hatua hiyo ya awali.

Taarifa hizo za kukamilika kwa ushahidi wa kesi hiyo zilipokewa kwa furaha na shangwe na msanii huyo, kiasi kwamba alishindwa kujizuia kuonyesha furaha yake.

Wakili wake Peter Kibatala aliiomba mahakama itoe ahirisho fupi hadi Ijumaa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa mashtaka haya mapya pamoja na maelezo ya awali.
Hakimu Mmbando alikubaliana na ombi hilo la Wakili Kibatala na akaahirisha kesi hiyo hadi Ijumaa.(CHANZO:MWANANCHI)

No comments:

Post a Comment