Saturday, December 22, 2012

DK.MWAKYEMBE ATIMUA WENGINE 16 BANDARI.


Dk Mwakyembe atimua wengine 16 Bandari

DAR ES SALAAM-TANZANIA 
Baada ya kuwasimamisha viongozi saba, akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Ephraim Mgawe, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, ameendelea na juhudi za kutaka kuirejeshea hadhi mamlaka hivyo, na safari hii amewasimamisha kazi viongozi wengine 16.
Dk Mwakyembe aliyasema hayo jana alipozungumza na wafanyakazi wa mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam, akisema uamuzi wake umekuja baada ya kubainika kuwepo kwa matatizo mengi yanayokwamisha ufanisi wa shughuli za mamlaka hiyo.
Alisema Bodi mpya ya TPA ilikutana na kupitia taarifa ya uchunguzi na baada ya kuipitia walichoamua ni pamoja na kuwasimamisha viongozi wengine 16 na kufanya jumla ya viongozi waliosimamishwa na kuandikiwa barua za kujieleza hadi sasa kufika 23.
Mwakyembe alisema hatua ya kuwasimamisha wengine itaendelea itakapobainika nao wamefanya makosa.
Alisisitiza kuwa, lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha hadhi ya bandari inarejeshwa na kuboreshwa zaidi baada ya kubainika kuwepo kwa mapungufu mengi yaliyosababisha kupungua kwa ufanisi wa shughuli za mamlaka hiyo.
Waliosimamishwa ni Mkurugenzi wa Uhandisi, Mhandisi Mwandisi Bakari Kilo, Meneja Uhandisi, Mhandisi Raymond Swai, Ofisa Mhandisi Mkuu, Mary Mhayaya, Mkurugenzi wa Mipango, Florence Nkya, Meneja Ugavi na Ununuzi, Bahebe Machibya na Meneja Kitengo cha Ununuzi (PMU), Theophil Kimaro.
Wengine ni Mkurugenzi wa TEHAMA, Ayoub Kamti, Meneja Makasha, Mathew Anthony, Mkurugenzi wa Mifumo ya Menejimenti,
Dk Maimuna Mrisha, Meneja TEHAMA, Marcelina Mhando, Ofisa Ulinzi, Fortunatus Sandaria, Kitengo cha Marine Fadhili Ngorongo, KOJ Opereta Owen Rwebangira, Diver Mohamed Abdullah na Opereta Kilimba.
Aliyataja baadhi ya mapungufu yaliyobainika kwa mujibu wa taarifa hiyo ya uchunguzi kuwa ni kuwepo mgongano wa kimaslahi ambapo viongozi wa ndani ya mamlaka hiyo wamekuwa na kampuni zao ndogo ndogo zinazohudumia bandari.
“Huwezi kuendeleza mamlaka ya bandari kwa mtindo huu. Kama una maslahi yako huwezi kusimamia shughuli za mamlaka ipasavyo. Kama hiyo haitoshi tumekwenda hadi Brela hizo kampuni hazijasajiliwa, ni za mfukoni tu,” alisema.
Alisema wote waliobainika kuwa na kampuni hizo wameandikiwa barua wajieleze, kwa nini wasichukuliwe hatua za kisheria. Katika hatua nyingine Waziri Mwakyembe ametoa onyo kwa wale wote walioingia katika ajira kwa mipango bila sifa wajiondoe wenyewe kabla hawajafukuzwa kazi.
Alisema moja ya kikwazo cha ufanisi katika mamlaka hiyo ni ajira kutolewa bila kufuata taratibu na Sheria za Nchi na kuonya kuwa wale wanaojijua wameajiriwa kwa mtindo huo waache kazi wenyewe ili walipwe mafao yao badala ya kusubiri kuachishwa na kupoteza kila kitu.
Waziri Mwakyembe pia alizungumzia tatizo la kukithiri vitendo vya wizi ambavyo alivielezea kuwa na mtandao mkubwa. Hata hivyo, alisema tatizo hilo litakomeshwa kabisa.
“Haiwezekani kuruhusu hali hii iendelee. Inakuwaje kontena nzima inayeyuka kama kiberiti, huu ni mtandao mkubwa lazima tuukomeshe kabisa,“ alisema.
Alisema inatia aibu kuona mapato ya Bandari ya Dar es Salaam kwa mwezi ni Sh milioni 27 hadi 28 kwa mwezi wakati Mombasa ni Sh bilioni tatu. Hata hivyo alisema tangu mwezi Septemba ufanisi mzuri umekuwepo hadi mapato yameongezeka.
“Wale walizoea mchezo huu wa kuchuma kwa njia ya wizi nitawakamata, pamoja na wale wanaoiba vitu humu ndani na kufanya biashara ya kuuza kwa kushirikiana na wale deiwaka wanaosimama hovyo kwenye kijiwe nje, nitawakamata pia,” alisema.
Alipiga marufuku utaratibu wa kulipisha mawakala Sh 200 kama pasi ya bandari (port pass) na badala yake ametaka mamlaka
kuweka utaratibu wa kudhibiti watu kuingia hovyo na kuhakikisha kila mmoja ana kitambulisho kinachoeleweka na anajulikana
anakwenda wapi na anakwenda kufanya kitu gani.(CHANZO:HABARI LEO)

No comments:

Post a Comment