Sunday, December 16, 2012

WANANCHI WAUA POLISI WAWILI KAGERA


KAGERA-TANZANIA,
WANANCHI wa Kata ya Mugoma, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera wamewaua askari polisi wawili na kuchoma moto Kituo cha Polisi Mugoma kwa madai kuwa polisi hao wamemuua kwa kumpiga risasi mwananchi mwenzao bila hatia.
Tukio hilo la lilitokea jana mchana wilayani humo na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi.
Akizungumza wakati akielekea eneo la tukio, Kamanda Kalangi alisema: “Tukio limetokea Kijiji cha Mugoma, sina details (maelezo ya kina), kwa sababu ndiyo nakwenda huko, ila nikifika ndipo nitajua nini kimetokea, nitatoa maelezo kwa kina.”
Habari zilizorushwa na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC), jana jioni zilieleza kuwa askari polisi waliouawa ni Koplo Pascal na Konstebo Alex wa Kikosi cha Usalama Barabarani wilayani Ngara.
Katika taarifa hiyo ya BBC, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Costa Kanyasu naye alithibitisha vifo vya askari hao na kueleza kuwa wanaendelea kufanya uchunguzi kujua ukweli wa tukio hilo, ikiwa ni pamoja na kujua kama askari hao ndiyo walimpiga risasi mwananchi huyo.
Ilidaiwa kuwa polisi hao walifika katika Kijiji cha Mugoma kwa lengo la kukagua pikipiki mbovu na zisizokuwa na usajili.
Walipokuwa katika ukaguzi huo walifika katika gereji moja na kukuta mmiliki wake akitengeneza pikipiki, wakamtaka aipeleke kituoni kwa maelezo kuwa ilikuwa mbovu.
Ilidaiwa kuwa fundi huyo aligoma kutekeleza amri hiyo na katika ubishi, polisi mmoja alimpiga risasi na kufariki dunia papohapo.
Kitendo hicho kiliamsha hasira kwa wananchi waliokuwa jirani na eneo hilo ambao walianza kujikusanya katika eneo la tukio.
Mmoja wa watu mashuhuda wa tukio hilo, Mwandishi wa Habari wa Redio Kwizera iliyopo wilayani Ngara, Joyce Ngalawa alisema kuona hivyo, polisi anayedaiwa kufyatua risasi alikimbia na kujificha katika nyumba iliyopo jirani na gereji hiyo, huku akimwacha mwenzake.
“Wananchi walimvamia yule askari aliyebaki pale gereji na kuanza kumkata kwa mapanga na kumpiga mawe hadi akafariki dunia,” alisema.
Alisema baada ya mauaji hayo, wananchi hao walikwenda katika nyumba aliyokuwa amejificha askari wa pili na kutishia kuichoma moto iwapo angegoma kutoka.
“Mmiliki wa nyumba ile baada ya kuona wananchi hao wanataka kuichoma moto nyumba yake, alimtaka askari huyo atoke nje. Alipotoka tu, wananchi walimvamia na kuanza kumpiga mawe na kumuua,” alisema.(CHANZO:MWANANCHI)

No comments:

Post a Comment