Sunday, April 15, 2012

CRDB yatoa mabilioni kusaidia ununuzi wa mazao


Bi Rose Mollel afisa Uhusiano wa CRDB akiwasilisha mada kuhusu ununuzi wa mazao katika moja ya semina huko mkoani Kagera

                                     
BENKI ya CRDB imetoa mikopo ya kununulia mazao yenye jumla ya sh. bilioni 690.5 mwaka jana ikiwa ni sehemu ya jitihada za Benki hiyo kusaidia sekta ya kilimo nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dkt. Charles Kimei ametangaza.
Akimuelezea Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuhusu shughuli za Benki hiyo ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam leo (Jumatano Aprili 4, 2012), Dkt. Kimei alisema CRDB pia itaendelea kuwasaidia kifedha wafugaji ili wanufaike na mifugo yao na uchumi wa taifa ukue.
Dkt. Kimei alisema kati ya fedha hizo za kununua mazao, Sh. Bilioni 161 ni kwa tumbaku; sh. bilioni 127 ni kwa pamba; sh. bilioni 120 kwa kahawa; sh. bilioni 37 kwa korosho na sh. bilioni 245 kwa mazao mengine mbalimbali.
Alisema pia kwamba CRDB imetoa mikopo kwa baadhi ya Halmashauri mbalimbali kwa ajili ya kujengea Shule za Sekondari na mikopo kwa Taasisi za Elimu kujengea majengo ya Vyuo Vikuu na kupima viwanja.
Mikopo mingine ni binafsi kwa baadhi ya wafanyakazi kujengea nyumba; kununua vyombo vya usafiri; kufanya biashara ndogondogo na vile vile imekopesha vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS)  mbalimbali.
CRDB, moja ya Benki kubwa nchini, iliyoanzishwa mwaka 1996, ina matawi 75 katika mikoa yote na katika Wilaya za Kahama, Bariadi, Geita, Karagwe, Tarime, Mbozi, Mbinga, Hai, Mpanda, Masasi, Kilosa, Bagamoyo na Kilombero.
Ina mashine za kuchukulia fedha (ATM) 180; mashine za kununulia bidhaa madukani (POS) 620, ubia na SACCOS 485 na inaongoza nchini kwa rasilimali, amana za wateja, mikopo na faida.
Miongoni mwa changamoto inazokabiliana nazo ni kutolipwa madeni na baadhi ya wadaiwa waliochukua mikopo kwa dhamana ya Serikali na kesi nyingi  zinazochukua muda mrefu za baadhi ya wadaiwa za zuio la Mahakama kwa Benki kuuza mali za dhamana ya mikopo.
Waziri Mkuu Pinda aliipongeza Benki ya CRDB kwa mchango wake, hasa wa kusaidia sekta ya kilimo na akaahidi kuwa Serikali itazifuatilia na kuzipatia ufumbuzi changamoto za benki hiyo.
(mwisho)  

No comments:

Post a Comment