Monday, April 23, 2012

VIONGOZI WA DUNIA WAKUTANA LONDON KUJADILI HALI YA SOMALIA.


LONDON, UINGEREZA.
Viongozi mbalimbali duniani wanakutana leo hii Mjini London Uingereza kujadili hatima ya Somalia. Viongozi hao wanakutana na viongozi wa serikali ya Somalia kutafuta namna ya kuunganisha nguvu dhidi ya Uharamia, Umasikini uliokidhiri, njaa na Vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia.
Takribani nchi 40 zimetuma wawakilishi katika mkutano huo huku Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi.Hillary Clinton na Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon wakiwa miongoni mwa wahudhuriaji.Wahudhuriaji wengine ni Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika, na Umoja wa Nchi za Kiarabu.

Hata hivyo kikundi cha waasi wa Al-Shabab kinachopigana kuipinga Serikali ya Somalia hakijawakilishwa katika Mkutano huo, huku kiongozi wake kamanda Abu Abudurehman akionya kuwa ikiwa matokeo ya mkutano huo yatakuwa ni uingiliaji wa mambo ya Somalia basi utapelekea hali mbaya zaidi nchini humo.
Uingereza ambayo ndiyo nchi mwenyeji na muandaaji wa mkutano huo imesema lengo la mkutano huo ni kukutanisha, na kuunganisha nguvu za pamoja za kimataifa juu ya Somalia.
Mkutano wa aina hii uliwahi kufanyika miaka 20 iliyopita na kupelekea kuongezeka kwa misaada ya kimataifa nchini Somalia ingawa haujafanikiwa kuleta mabadiliko makubwa mpaka sasa.
Somalia imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mingi tangu kuangushwa kwa Utawala wa kiditekta wa Bw.Siad Barre mwaka 1991, ambapo kwa mujibu wa Shirika la msalaba mwekundu zaidi ya watu Milioni Moja wameuawa kutokana na vita hiyo.
Kwa sasa Nchi hiyo ina serikali dhaifu chini ya Rais Sheikh Sharif Sheik Ahmed ambayo inadhibiti baadhi ya maeneo tu ya nchi hiyo huku ikikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa kundi la Al-shabab.
Lengo kuu la mkuatano huo litakuwa ni Usalama, njaa, lakini kitu muhimu ni nini kitafuata baada ya mkutano huo ikizingatiwa kuwa serikali iliyopo madarakani ilishamaliza muda wake tangu mwezi Agosti mwaka jana.Pengine wasomalia wasubiri nini kitaamuliwa kwani labda wakati huu kunaweza kuwa na matumaini na hali ikawa tofauti na yale yaliyojiri baada ya lundo la mikutano iliyokwishafanyika juu ya Somalia.


No comments:

Post a Comment